Za Chembe Lazima Ukae
Ojuku Abraham, +255 719 786 355
MIAKA kadhaa ya kufanya kazi na watu
wenye majina makubwa, wenye mamlaka na walio katika nafasi nyeti, imenipatia
funzo kwamba unapaswa kuwa makini sana kwa nyendo zako, kama lengo lako ni kuwa
mtu maarufu, lakini mwenye hadhi katika jamii.
Unapokuwa mtu maarufu, unachukuliwa kama mfano na
bahati mbaya, mfano ni mfano tu, uwe mbaya au mzuri. Mtu anaweza kumwambia
mwanaye kwa mfano, asiwe malaya kama Kim Kardansian, yule dada mrembo mwenye
msururu wa wanaume aliotokanao huko Marekani. Ni staa mkubwa lakini mwenye sifa
mbaya, licha ya hivi sasa kuwa mke wa Kanye West.
Na mtu mwingine anaweza kukuambia kuwa wapaswa
kuwa na nidhamu, heshima na utu kama Ronaldo de Lima, mwanasoka nyota aliyepata
kila aina ya mafanikio uwanjani, akishinda mataji yote makubwa ya soka duniani,
lakini akibakia kuwa muungwana uwanjani, mpole nje ya uwanja na mwenye utu
katika maisha ya kijamii.
Umaarufu unakufanya uwe mtu wa kutazamwa kwa kila
unachokifanya. Watu wataulizana, hivi fulani ameoa? Ana watoto wangapi, maisha
yake yakoje, anapendeleaga nini na mambo mengine chungu nzima. Na mara nyingi,
umaarufu unapatikana kupitia kazi tunazofanya.
Lakini umaarufu huu nao umegawanyika, ule wa sifa
mbaya na ule wenye hadhi. Tunao mastaa ambao siku zote tunategemea kusikia juu
ya skendo na inapotokea wakatokea kwenye shughuli zenye heshima, kila mmoja
huidharau hafla hiyo. Hawa wapo na wote tunawajua.
Lakini wapo baadhi ya mastaa wetu ambao inakuwa
vigumu kidogo kuamini tunaposikia habari mbaya zinazowahusu, hata kama ni kweli
wamefanya kinachosemwa. Hii ni kutokana na jinsi wao wenyewe walivyojitengeneza
katika umaarufu wao.
Enzi zile nikikua, kulikuwa na jambazi mmoja
maarufu sana jijini Dar es Salaam, akiitwa Nyau. Habari zake zilitingisha kila
kona na kila mmoja aliogopa kukutana naye. Ziliposikika habari kwamba ameuawa,
kila mpenda amani alifurahi. Unapoona watu wanafurahia anguko lako, ni dhahiri,
maisha yako yalikinzana na matazamio yao!
Kwa nini nimesema hivi, ni kwa sababu uzoefu
wangu kwa miaka niliyojihusisha na mastaa, unanionesha kuwa wapo baadhi yao
hawajui namna ya kuishi katika hadhi waliyonayo, wengi wao wakitumia ustaa wao
kujinufaisha kwa njia zisizofaa na wachache, wakiishi hasa maisha yenye kwenda
sawia na hadhi waliyojijengea.
Wapo watu wanaotafuta majina makubwa ili wafanye
utapeli na umalaya. Lengo lao ni kutumia umaarufu wa majina yao ili kufanikisha
lengo lake. Bahati mbaya inakuja pale anapoitumia fani kutimiza lengo lake,
matokeo yake ni kuonekana watu wote walio katika industry kuwa ni wenye sifa
kama zake.
“Unataka kuwa muigizaji, achana na hiyo fani,
wasichana wa Bongo Movie ni malaya,” mtu mmoja anaweza kumwambia binti
anayejaribu kupenyeza ili awe muigizaji, aweze kutimiza ndoto zake za muda
mrefu.
Hii haimaanishi kweli kuwa Bongo Movie ni chaka
la wahuni, isipokuwa kwa sababu mtu mmoja au wawili, wameitumia fani hiyo
vibaya. Watu wengine wamejaribu kuwa wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, dansi
au taarab, wakiamini huko kunaweza kupata umaarufu.
Ninajua wapo wasanii wenye majina makubwa, lakini
wanayatumia vizuri kuchangamkia fursa zinazokuja mbele yao, hawa sina tatizo
nao. Lakini sipendezwi zaidi na matapeli au malaya wanaotumia fani kutekeleza
matakwa yao.
Rai yangu ni kwa jamii zinazohusika, kuwakataa
watu hawa kuwa miongoni mwao. Tusikubali matapeli wajineemeshe kwa majina
wanayoyapata kupitia fani zetu. Uzuri ni kuwa tunajuana, tunafahamu kuwa huyu
anaishi kwa sababu ya utapeli au wanaume, fani ni kigezo tu, tumkatae!
0 comments:
Post a Comment