Undani mwanajeshi alivyomuua mkewe kwa panga


Marehemu Rudia Joseph enzi za uhai wake.
         
Stori: Makongoro Oging’ na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Vilio, majonzi bado vimetawala Mtaa wa Kirezange, Kata ya Kivule Wilaya ya Ilala, Dar kufuatia mauaji ya kikatili ya Rudia Joseph yanayodaiwa kufanywa na mumewe, Joseph Mahende ‘Thang’ana’ ambaye ni askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kambi ya Lugalo, Dar.

Rudia aliaga dunia kutokana na majeraha makubwa yaliyosababishwa na kukatwa mapanga mwilini usiku wa kuamkia Jumatatu, wiki iliyopita.

UWAZI LACHIMBA
Baada ya mauaji hayo, Uwazi lilitinga eneo la tukio ili kuchimba kwa kina ambapo lilifanikiwa kuzungumza na majirani.




Waombolezaji wakiuaga mwili wa marehemu kwa ajili ya kusafirishwa.

Uwazi lilikuta mwili wa marehemu umepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili huku mtuhumiwa akiwa Kituo cha Polisi Stakishari, Dar baada ya kujipeleka mwenyewe.

Kwa mujibu wa majirani, walisikia kelele za mwanamke huyo akiomba msaada wakati akikatwa mapanga, lakini waliogopa kuingia ndani kusaidia kwa vile walijua mwanajeshi huyo angewageuzia kibao.

SIMULIZI YA MPANGAJI
Mpangaji wa mwanajeshi huyo, Hellana Mtega aliyekuwepo siku ya tukio, katika mahojianao na Uwazi kuhusu mauaji hayo, alisema:
“Nyumba hii tupo wapangaji watatu wa kike, lakini leo tuko wawili. Tunaishi na mwanajeshi na mkewe.

Mwili wa marehemu ukiandaliwa .

“Iikuwa saa 5:30, usiku walipoanza ugomvi wa maneno. Kilichoonekana ni kwamba, mwanaume alikuwa akimshutumu mkewe kwa kitendo cha kwenda kazini kwake Lugalo na kutaka awe anapokea nusu mshahara wa mumewe akidai hahudumiwi, hivyo anakula jasho lake bure.

“Kutokana na ugomvi huo, marehemu aliamua kwenda sebuleni. Sisi hatukushangazwa mzozo wao kwani ni wa mara kwa mara, hata majirani zetu wanajua.”

MTUHUMIWA KABLA YA KUKUMBWA NA MADAI
“Jana jioni, kuna baa jirani ambapo mwanajeshi anapenda kunywa. Nasikia alikwenda akalipa madeni yote aliyokuwa akidaiwa. Aliporudi kwake, akalala, baadaye, saa 5:30 usiku ndipo ugomvi ukaanza. Basi, baada ya mke kwenda sebuleni, alimfuata akiwa na mti wa fagio na kuanza kumpiga nalo. Alifunga mlango wa nje kwa kufuli.

“Wakati huo marehemu alikuwa akipiga kelele ili asaidiwe lakini mimi na mpangaji mwenzangu tulikuwa tukichungulia tu dirishani. Kwa kweli tulishindwa kumsaidia kwani tabia ya mwanajeshi kila mmoja anaijua, ni mkali sana.”

KIPANDE CHA CHUMA
“Baadaye, mwanajeshi alichukua kipande cha chuma na kuanza kumponda nacho mkewe. Mimi niliumia sana kwa kweli, nikaamua kumfungulia mlango wa chumba changu ili aingie kisha niufunge. Lengo likiwa mumewe asiendelee kumpiga.

Jeneza likibebwa kwa ajili ya kupakizwa kwenye gari.

“Lakini mwanajeshi alinionesha panga na kunitaka niondoke haraka la sivyo angenikata. Wakati huo mkewe aliendelea kupiga mayowe, hakuna hata mtu aliyejitokeza kumsaidia.”

SAUTI YA MWANAJESHI
“Baadaye nikamsikia mwanajeshi akisema, ‘ngoja nikufungulie mlango ukafie nje.’ Marehemu baada ya mlango kufunguliwa alikimbia nje ili kujiokoa lakini kwa bahati mbaya akateleza, akaanguka. Mumewe aliendelea kumpiga kwa kile kipande cha chuma, akaishiwa nguvu, akawa anatweta.”

MWANAJESHI ALICHUKUA KITI
“Kwa kuona mkewe ameanguka, mwanajeshi alichukua kiti na kwenda kukaa karibu naye huku akimwambia maneno ambayo sikuyaelewa kwani alikuwa akizungumza kilugha. Ndipo baadaye alichukua panga na kuanza kumkatakata. Baada ya hapo hatukusikia tena kelele za mwanamke.”

MWANAJESHI APIGA DEKI
“Baada ya kuona mkewe amefariki dunia, mume alirudi ndani, akadeki ili kuondoa damu. Kisha akamwita mtoto wake wa kiume wa mke mwingine maana marehemu hakuzaa naye.

“Alimwambia mwanaye anataka kujiua kwa vile ameua, mwanaye alimkataza na kumpigia simu baba yake mkubwa (kaka wa mwanajeshi) ambaye anaishi karibu. Alifika mara moja na kumsihi mwanajeshi asijiue bali akajisalimishe kituo cha polisi.”
Jeneza lililobeba mwili wa marehemu likipakizwa kwenye gari.

MWANAJESHI APANDA BODABODA
“Alipanda bodaboda, akaenda Kituo cha Polisi Stakishari kujisalimisha. Kwa mujibu wa maelezo ya askari mmoja, alipofika alijitambulisha, akawataka polisi wamfungulie mlango wa mahabusu kwa kuwa ameua lakini walimkatalia.”

POLISI WAMPA MAELEKEZO
“Polisi walimwambia kama kweli ameua aende kwa mjumbe wake ampe barua kisha arudi nayo kituoni. Alifanya hivyo, alimfuata mjumbe wetu, akamweleza hali hiyo lakini naye akashangaa. Alimwambia kama haamini waongozane akashuhudie. Walifutana hadi hapa na kushuhudia maiti.

“Ndipo mjumbe akamwandikia barua na kumgongea mhuri, mwanajeshi akapanda tena bodaboda hadi Stakishari na kuonesha ile barua kwa polisi, ndipo walipoamini na kumfungulia mlango wa mahabusu. Polisi walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili.”

KAULI YA MJUMBE
Mjumbe wa Shina Namba 17 Kata ya Kivule, Jackson Mathayo Chacha alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema mwanajeshi huyo alikuwa na ugomvi wa kifamilia na marehemu na alikuwa akiwasuluhisha mara kwa mara. Pia, alikiri mwanajeshi huyo kurudi kutoka Polisi Stakishari kuhitaji barua ambapo alimpatia.



Waombelezaji wakiwa msibani.

KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, SACP Lucas Mkondya alikiri kutokea kwa mauaji hayo: “Ni kweli mauaji hayo yametokea na mtuhumiwa Joseph Mahende tunamshikilia huku upelelezi ukiendelea,” alisema.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, marehemu alikuwa mke wa tatu kati ya wanne wa mtuhumiwa. Mwili wake ulisafirishwa Jumatano iliyopita kwenda Serengeti, Mara kwa mazishi.


globalpublisher
Next PostNewer Post Previous PostOlder Post Home

0 comments:

Post a Comment